Tanzania imeahidiwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kuungwa mkono katika vipaumbele vya mazingira ikiwemo agenda ya nishati safi ya kupikia.
Hayo yamejiri wakati wa mazungumzo kati ya Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme amekutana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Bi. Elizabeth Mrema Julai 11, 2024 jijini Nairobi, Kenya.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika kikao cha pembeni baina ya viongozi hao wakati wa Mkutano wa 11 wa Wawakilishi wa Kudumu wa UNEP uliotarajiwa kumalizika Julai 12, 2024.
Bi. Mndeme ameishukuru UNEP kwa kuisaidia Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye lengo la kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Halikadhalika, ameliomba shirika hilo kuendelea kuunga mkono Tanzania hususan katika utekelezaji wa vipaumbele vya nchi katika sekta ya mazingira vikiwemo agenda ya nishati safi ya kupikia, biashara ya kaboni na uchumi wa buluu.
Bi. Mrema ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa michango yake kwenye agenda zilizowasilishwa na kujadiliwa kwa kipindi chote cha mkutano huo.
Kutokana na hatua hiyo Naibu Mkurugenzi huyo amepokea michango hiyo na kuahidi kuichukua kwa ajili ya kuweka kwenye vipaumbele kwenye mpango kazi wa Shirika la UNEP katika kipindi cha mwaka 2024-2025 kwa ajili ya kuifanyia kazi.
Mkutano wa 11 wa Wawakilishi wa Kudumu wa UNEP unafanyika kwa lengo la kupitia programu za shirika hilo UNEP kwa kipindi cha mwaka 2022- 2023 na kupitia mpango kazi na bajeti kwa mwaka 2023 – 2024.
Pia, katika mkutano huo wajumbe wanapitia utekezaji wa kazi za shirika hilo hususan kwenye masuala ya mabadiliko ya tabianchi, bioanuwai na uchafuzi wa mazingira.
Sanjari na hayo, pia wajumbe wa mkutano huo uliofunguliwa Julai 08, 2024 wamepata wasaa wa kufanya maandalizi ya mikutano ijayo ya Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA – 7).
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umewakilishwa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme na Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. Bernad Kibesse.