Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika ukanda huo.
Hayo yameelezwa Desemba 11, 2024 Jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi Christina Mndeme wakati wa mazungumzo baina yake na Ujumbe wa Wizara ya Maliasili na Mabadiliko ya Tabianchi wa Serikali ya Jamhuri ya Malawi ulioongozwa na Mkurugenzi wa Mazingira wa Wizara hiyo, Bi. Tawonga Mbale-Luka.
Mndeme amesema mataifa mbalimbali kwa sasa yanakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ongezeko la joto, mvua zisizotabirika na mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa na hivyo kuhitajika kwa nguvu za pamoja za kukabiliana ikiwemo kuimarisha ushirikiano wa kikanda baina ya mataifa.
Ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa ushirikiano na Jumuiya za Kimataifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambapo Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris.
“Jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabainchi zimeibua changamoto na fursa muhimu ambazo zinaweza kusaidia Tanzania katika kuchochea uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu ikiwa ni pamoja na kufanya mapitio ya sera, uandaaji wa kanuni, mikakati na miongozo” amesema Mndeme.
Aidha ameongeza kuwa Biashara ya Kaboni ni mojawapo ya nyenzo muhimu katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi duniani, hivyo pamoja na sera na mikakati iliyopo Serikali imeandaa Kanuni na Mwongozo wa Taifa wa Usimamizi wa Biashara ya Kaboni nchini ili kuinufaisha jamii.
Amefafanua kuwa Kanuni na Mwongozo wa Usimamizi wa Biashara ya Kaboni zimejikita katika kuimarisha mchango wa nchi katika jitihada za kupunguza uzalishaji wa gesijoto na kuzingatia misingi ya ushiriki wa jamii, uwazi na uzingatiaji wa viwango vya kimataifa.
Kwa mujibu wa Mndeme, Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ipo tayari kushirikiana na Malawi katika kuunga mkono juhudi za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kujenga uwezo wa kitaalamu na kubadilisha uzoefu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Serikali ya Jamhuri ya Malawi, Bi. Tawonga Mbale-Luka ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kukubali mwaliko wa nchi hiyo kufika nchini na kujifunza masuala ya usimamizi wa mabadiliko ya tabianchi na biashara ya kaboni.
Ujumbe wa Wizara ya Maliasili na Mabadiliko ya Tabianchi wa Serikali ya Jamhuri ya Malawi upo nchini kwa ziara ya Siku nne ambapo unatarajia kutembelea Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kilichopo Mkoani Morogoro.