Tanzania Kituo bora cha Mawasiliano ya Dharura

Tanzania imeendelea kutolewa mfano wa kuwa na Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura (National Emergency Operation and Communication Center Situation Room) na kuelezwa kuwa nchi nyingine ziendelee kuiga mfano wa Tanzania na kuendelea kuwekeza katika mifumo ya tahadhali za mapema -early warning systems kwa kutumia vyanzo vya ndani, kushirikisha jamii na sekta binafsi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ameyasema hayo 13 Novemba, 2024 wakati wa Mkutano wa 29 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaoendelea mjini Baku, nchini Azerbaijan.

Dkt. Yonazi amesema kuwa,Tanzania imeendelea kuwa kinara katika masuala ya menejimenti ya maafa hususan katika kuzuia, kupunguza kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea, huku akitaja mafanikio ya uwepo wa kituo cha ufuatiliaji wa majanga (situation room) ikiwemo ya kurahisisha ufuatiliaji wa mwenendo wa janga lililotabiriwa na kufanya uchambuzi wa kiwango cha madhara kwa jamii, miundombinu na mazingira.

Pia kituo hicho kimesaidia kuandaa taarifa za tahadhari ya mapema ya hatua za kuchukua ili kuzuia, kujiandaa na kukabili maafa, kuandaa taarifa ya mwenendo wa tukio na kusambaza kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kusaidia uratibu na utekelezaji wa shughuli za kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wadau kuwezesha utekelezaji wa afua za usimamizi wa maafa katika eneo la mifumo ya tahadhali ya mapema.

Dkt. Yonazi ametumia jukwaa hilo kuyakaribisha Mataifa mbalimbali kuja kujifunza Tanzania namna Kituo hicho kinavyofanya kazi katika kuratibu mwenendo wa majanga kwa umahiri wa hali ya juu.

“Uwepo wa kituo hiki umewavutia wadau wengi kuja kujifunza huku wengine wakiahidi kuunga mkono juhudi za Tanzania katika masuala ya menejimenti ya maafa,” alisema Dkt. Yonazi.

Related Posts