TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU USHIRIKI WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA KIMATAIFA WA MABADILIKO YA TABIA NCHI (COP 28) ULIYOFANYIKA DUBAI, UMOJA WA FALME ZA KIARABU KUANZIA 30/11/2023 HADI 12/12/2023
UTANGULIZI
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) imeshiriki katika Mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) uliofanyika Dubai Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 30 Novemba hadi tarehe 12 Desemba, 2023.
LENGO LA COP28
Lengo la COP 28 ni kupitia taarifa, kufanya kutathmini, majadiliano na maamuzi kuhusu hatua zilizochukuliwa na nchi wanachama katika kufikia malengo ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto pamoja na Makubaliano ya Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi. Ujumbe Mkuu wa COP 28 ilikuwa “Unite, Act, Deliver”. Kauli mbiu hii ililenga kuzitaka nchi wanachama wa Mkataba kuungana na kutekeleza kwa pamoja sera, mipango na mikakati ya mabadiliko ya tabianchi. Mkutano huu ulihudhuriwa na washiriki takribani 110,000.
AGENDA ZILIZOJADILIWA
Agenda zilizojadiliwa katika kutano wa COP28 ni pamoja na Lengo la dunia la Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi; Tathmini ya Kidunia ya Utekelezaji wa Makubaliano ya Paris;Utekelezaji wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi na Mipango ya Taifa ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi; Hatua wezeshi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi; Upatikanaji wa rasilimali fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi; Uendeshaji na uwezeshaji wa Mfuko wa hasara na uharibifu yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kuanza kufanya kazi; Mfumo wa masoko na usio wa masoko wa biashara ya kaboni; Utekelezaji wa Programu ya Sharma Sheikh kuhusu kilimo na mabadiliko ya ya tabianchi;Kujenga Uwezo wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi; Kuimarisha utekelezaji wa hatua za kupunguza uzalishaji wa gesijoto;Utekelezaji wa Ibara ya Sita ya Makubaliano ya Paris kuhusu Mfumo wa Masoko na usio wa masoko katika kukabiliana mabadiliko ya tabianchi; Mfumo wa uwazi katika mikakati na misaada inayotolewa; Uendelezaji na uhaulishaji wa teknolojia na Athari za hatua za sera za kitaifa na kimataifa.
USHIRIKI WA TANZANIA
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) uliongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Viongozi wengine walioambatana na Mheshimiwa Rais walikuwa ni Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge, Makatibu Wakuu, Wataalamu na Wawakilishi kutoka Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia. Kwa upande wa Tanzania jumla ya washiriki 50 kutoka Serikalini ikiwemo Wizara, Idara na Taasisi za Serikali (SJMT), Wabunge 3; washiriki 8 kutoka SMZ na 300 kutoka sekta binafsi, Asasi za Kiraia ikiwemo vijana na Watoto walishiriki.
Kauli Mbiu ya Kitaifa, ambayo ujumbe wa JMT ilikwenda nayo ilikuwa ni “Kuimarisha Hatua za Kilimo Himilivu na Uchumi wa Bluu”. Kauli Mbiu hii ililenga Kuchochea Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa kuwa na Kilimo Endelevu, na kutumia vizuri fursa za Uchumi wa Buluu.
Msimamo wa Taifa, Katika kuwezesha ushiriki kikamilifu, Tanzania iliandaa Msimamo wa Taifa ambao ulisaidia kuongoza Dira ya ushirikiri na majadiliano ya wajumbe wa Tanzania. Msimamo huo uliandaliwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali ikiwemo wizara, idara na taasisi za serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na asasi za kiraia kwa kuzingatia sera, mipango, mikakati na programu za kitaifa za Tanzania Bara na Zanzibar.
JENGO LA MAONESHO
Sanjari na mikutano hiyo SJMT ilikuwa na jengo la maonesho pamoja na ofisi katika mkutano huu ambapo jumla ya washiriki 4,700 walitembelea jengo hilo ili kujionea jitihada mbalimbali zinazotekelezwa na nchi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
MKUTANO WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI
Mkutano wa 28 ulitanguliwa na Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali (World Leaders Action Summit) uliyofanyinyika tarehe 1-2 Disemba 2023 na kufuatiwa na vikao vya majadiliano katika ngazi kamati mbalimbali za kitaalam. Mkutano huu ulihudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali takribani 176. Mkutano ulifunguliwa tarehe 1 Desemba, 2023 chini ya uenyekiti wa Mhe. Dkt. Sultan Ahmed Al Jaber, Rais wa COP28. Katika hotuba yake ya ufunguzi, Dkt. Al Jaber alipongeza uamuzi wa nchi wanachama kufikia uamuzi wa kuanza utendaji kazi wa mfuko wa kukabiliana na uharibifu na upotevu unaotokana na mabadiliko ya tabinchi (Loss and Damage Fund) na kueleza kuwa tayari nchi mbalimbali zimeahidi kuchangia fedha taslim kwenye mfuko huo na kuahidi kuratibu jitihada za kufikia lengo la kupunguza uzalishaji wa gesi joto kufikia nyuzi joto 1.5. Mkutano huu ulihudhuriwa pia na Mhe. Antonio Guteres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mfalme wa Uingereza Charles III
Pamoja na kufunguliwa kwa mkutano huo,tarehe 01/12/2023 Mhe. Dkt. Samiua Suluhu Hassan alipata fursa ya kuhutubia Wakuu wanchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) na kutoa Tamko la Nchi kupitia hotuba hiyo. Katika hotuba yake Mheshimwa Rais alisema kuwa “Jijini Copenhagen, Denmark nchi zilizoendelea ziliahidi kutoa Dola za Kimarekani bilioni 100 kila mwaka kwa nchi zinazoendelea ifikapo mwaka 2020 ingawa kiasi hiki bado hakitosherezi na hakijafikiwa ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, Jijini Paris, Dunia iliazimia na kuweka lengo la upunguzaji wa ongezeko la joto duniani chini ya nyuzi joto 1.5 ifikapo mwaka 2030 licha ya kuwa kiwango cha joto duniani kwa sasa kinatishia usalama wa dunia, viumbe hai na mifumo ikolojia. Ni lazima ieleweke kuwa, ahadi ambazo hazijatekelezwa huondoa mshikamano na uaminifu, na kuwa na matokeo yasioridhisha na ya gharama kubwa kwa nchi zinazoendelea. Tanzania inapoteza asilimia 2 hadi 3 ya Pato la Taifa kutokana na mabadiliko ya tabianchi”.
Masuala mengine ambayo Mheshimiwa Rais aliyazungumuza katika hotuba yake ni kuwa Ripoti ya Jopo la Kisayansi Duniani ya mwaka 2023 imetoa tahadhari kuwa “hatua zilizopo za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hazitaweza kupunguza ongezeko la joto duniani. Hivyo kuweka Mwongozo wa lengo la pamoja la Kidunia wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ni suala la haraka na siyo kuchagua. Uamuzi ni wetu: kuzingatia sayansi ya mabadiliko ya tabianchi au kuacha athari za mabadiliko ya tabianchi zituathiri”.
MIKUTANO YA PEMBEZONI YA NGAZI YA JUU
Pamoja na mikutano hiyo, SJMT imeshiriki mikutano ya pembezoni ya ngazi ya Juu, Mikutano ya pembezoni na mikutano ya uwili. Mikutano ya pembezoni ya ngazi ya juu iliyoendeshwa na Tanzania ilihusu:
Uzinduzi wa Mpango wa kukuza matumizi na nishati safi na nafuu ya kupikia kwa wanawake barani Afrika; Mkutano huu ulihudhuriwa na wadau walioshiriki ana kwa ana zaidi ya 150, na wengine wakishiriki kwa njia ya mtandao. Wadau walioshiriki ni pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Afrika ya Kusini na Burundi; Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Rwanda na Zimbabwe; Mawaziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway na Ufaransa; Wakuu wa Taasisi za Kimataifa ikiwepo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB); SNV; Care International; Jukwaa la Nishati Safi ya Kupikia Duniani (Clean Cooking Alliance – CCA); Taasisi za Kimataifa za Nishati za ENERGIA na IEA; Mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN WOMEN); Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF); Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP); Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO); Mpango wa Chakula Duniani (WFP); na wahisani akiwemo Mwakilishi wa Bloomberg L.P.
Kwa upande wa Tanzania, Mkutano ulihudhuriwa na Mawaziri na Makatibu Wakuu kutoka katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha, Nishati, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, na Maji;Wabunge; Mabalozi; na Wataalam wa Serikali na sekta binafsi.
Matokeo ya Mkutano huo ni pamoja na Mheshimiwa Rais kueleza masula muhimu kuhusu programu husika na mambo mbalimbali yanayohusu nishati safi ya kupikia barani Afrika hususan kwa wanawake ikiwemo: Umuhimu wa kuwawezesha wanawake na wasichana kutumia nishati na teknolojia safi za kupikia barani Afrika ili kupunguza athari za uharibifu wa mazingira, kuokoa afya zao na kuwawezesha kiuchumi. Aidha alisitiza malemgo mahussi ya Programu ikiwemo: Uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuchochea mabadiliko ya kisera barani Afrika; Utoaji wa mafunzo kwa wanawake kuhusu matumizi ya teknolojia safi za kupikia, ujasiriamali na uongozi pamoja na kuendeleza tafiti na teknolojia fanisi na nafuu za kupikia.
Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) ambao ni wadau wa nishati safi ya kupikia,wameonesha nia ya awali ya kusimamia rasilimali fedha za Programu ya AWCCSP; na Utekelezaji wa Programu utafanyika kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kusambaza nishati na teknolojia safi za kupikia ikiwemo majiko banifu na usambazaji wa umeme vijijini.
Kwa upande mwingine Wageni waalikwa wakiwemo Viongozi mbalimbali barani Afrika walitoa maoni kuhusu Progarmu husika ikiwemo Mhe. Cyril Ramaphosa, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini; alitoa uzoefu wa namna Afrika Kusini ilivyoweza kufanikiwa kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia kukuza matumizi ya nishati ya umeme. Pia, alifahamisha kuwa kipaumbele sasa nchini Afrika Kusini ni kukuza matumizi ya nishati jadidifu.
Aidha, Dkt. Akinwumi Adesina, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika; alieleza kuwa kutatua changamoto ya matumizi ya nishati ya kupikia kwa wanawake barani Afrika kunahitaji uwekezaji wa Dola za Marekani Bilioni 4 kila mwaka. Alisisitiza ili kufanikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa asilimia 100 barani Afrika ni muhimu kila Serikali kuwekeza katika suala hili, kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa kuboresha miundombinu ya kuzalisha, kuhifadhi na kusambaza gesi, Taasisi za kifedha kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kusambaza nishati safi ya kupikia na sekta binafsi ipatiwe ruzuku kuweza kusambaza nishati safi ya kupikia. Dkt. Adesina aliahidi kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika iko tayari kuungana na wadau wengine muhimu ikiwemo UNCDF kutafuta rasilimali fedha ili kuhakikisha Programu ya AWCCSP inafanikiwa.
Mhe. Monica Mtsavangwa, Waziri wa Masuala ya Wanawake na Maendeleo ya Jamii-Zimbabwe;akimuwakilisha Mheshimiwa RaisEmmerson Mnagangwa, alieleza kuwa uwekezaji katika masuala ya nishati safi ni jambo linalowezekana na rahisi, na limekuja kwa wakati sahihi. Hivyo amewasihi wadau kuchukua fursa hii kwa pamoja kuwainua wanawake na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, ambayo isiishie katika majadiliano pekee bali iwe ni miongozo ya msingi katika utendaji wao wa kila siku.
Hatua inayofuata ni pamoja na: Kukamilisha taratibu za makubaliano ya Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (United Nations Capital Development Fund- UNCDF) kusimamia rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza Programu ya AWCCSP; Kuandaa Mkutano wa Wataalam kwa ajili ya kujadili muundo wa utekelezaji wa Programu ya AWCCSP; na Kufuatilia ahadi za misaada ya hali na mali zilizotolewa na viongozi mbalimbali wakiwemo Marais wa nchi za Afrika, Mawaziri na Wakuu wa Taasisi za Kimataifa.
Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu fursa za uwekezaji kwenye sekta ya kilimo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (Kilimo) (Agricultural Opportunities for Green Growth Transformation in Tanzania)
Mkutano huu ulifunguliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, Mkutano ulihusisha Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Januari Makamba (Mb), Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais – Zanzibar Dkt. Omar Shajak na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Amina Shaaban. Baadhi ya Wadau wa Maendeleo na washirika muhimu walioshiriki katika mkutano huo walikuwa ni Mhe. Hailemariam Dessalegn, Waziri Mkuu mstaafu wa Ethiopia; Dkt. Beth Dunford, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika; Rodgers Voorhies, Rais wa Shirika la Global Growth and Opportunity at BMG Foundation na Martin Van Nieuwk, Mkurugenzi wa Dunia wa Benki ya Dunia , Benki ya Maendeleo ya Afrika, AGRA, IFAD, Wakurugenzi kutoka Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais – Zanzibar, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Masuala yaliyojadiliwa katika Mkutano huo ni mikakati ya Kukusanya kiasi cha Dola za Kimarekani 1.8 Bilioni kwa ajili ya kuchimba visima 65,000 (Adaptation measure) ambapo kila kisima kimoja kitahudumia wakulima 16 wenye mashamba ya ukubwa wa hekta 2.5.
Wadau wa Maendeleo waliahidi kuchangia programu hii kiasi cha Dola za kimarekani Milioni 610. Wadau wa maendeleo walioahidi kuchangia ni: World Bank USD Milioni 300; Africa Development Bank (AfDB) USD Milioni 100; AGRA USD Milioni 50; IFAD USD Milioni 60; USAID USD Milioni 100; AfDB imekubali kuwa mtafutaji fedha (Fund Mobilizer) kuhakikisha upatikanaji wa fedha za uchimbaji wa visima 65,000. Programu hii itasaidia uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya Kilimo na itapunguza uharibifu wa mazingira. Aidha, program hii itaongeza pato la mkulima kwa kuwa kila mkulima atakuwa na uwezo wa kulima zaidi ya mara moja kwa mwaka na vilevile programu hii itawanufainsha wakulima wadogo takribani millioni 2.04. Hatua inayofuata ni Kufuatilia ahadi zilizotolewa na kuendelea kuhamasisha wadau wengine kuchangia programu hii.
Mkutano wa Kuongeza kasi ya kupambana na mabadiliko ya Tabianchi katika sekta ya kilimo kwa kushughulikia hasara na uharibifu unaotokana na athari mabadiliko ya Tabianchi (Accelerating climate smart innovation in Agriculture by addressing loss and damage innovative sources of finance).
Mkutano huu ulifunguliwa na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb). Wadau wengine walikuwa ni pamoja na Dkt. Beth Dunford- Makamu wa Rais Benki ya Maendeleo Afrika; Bw. Martien van Nieuwkoop World Bank Global Director for the Agriculture; na Waziri wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi wa UAE.
Matokeo ya Mkutano huo ni pamoja na mapendekezo mbalimbali yalitolewa ya namna ya kukabiliana na athari za mabaliko ya tabianchi ikiwemo: kuimarisha utafiti katika Sekta ya Kilimo kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi kama vile kutambua aina za mbegu zinazostahimili ukame na mafuriko; kuwekeza katika teknolojia zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi; kuweka mazingira wezeshi ya kisera ili kuvutia uwekezaji zaidi; na kuendelea kuimarisha mashirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi; na Shirika la CARE International kuendelea kufanya kazi na Serikali na wadau wengine kwa pamoja katika kutafuta suluhu ya athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia programu mbalimbali.
Mkutano wa Reaching the Last Mile Forum
Mheshimiwa Rais alishiriki kwenye Mkutano wa Reaching the Last Mile Forum uliofanyika tarehe 3 Desemba 2023, siku mahususi iliyotengwa kwenye COP28 kujadili uhusiano kati ya masuala ya afya na mabadiliko ya tabianchi. Mkutano huo ulihudhuriwa na Bwana Bill Gates, Mwanzilishi Mwenza wa Taasisi ya Bill na Melinda, Wawakilishi wa Marais wa Umoja wa Falme za Kiarabu na Sierraleone, Mawaziri kutoka nchi mbalimbali na wahisani. Lengo la Jukwaa hilo lilikuwa ni kuchagiza upatikanaji wa rasilimali fedha, kwa ajili ya Mfuko unaotarajiwa kuwa wa kiasi cha Dola za Marekani Milioni 500, ili kusaidia juhudi za nchi mbalimbali katika kutokomeza magonjwa yaliyosahaulika ya maeneo ya tropiki (Tropical Neglected Diseases), hususan river blindness na lymphatic filariasis barani Afrika katika kipindi cha miaka saba kuanzia2023 hadi 2030. Mheshimiwa Rais alieleza kuwa miaka kumi iliyopita, magonjwa ya river blindness na lymphatic filariasis yalikuwa ni tishio nchini Tanzania hata hivyo, kwa sasa magonjwa hayo yameweza kudhibitiwa kupitia jitihada za nchi na wadau wa maendeleo ikiwemo nchi za Marekani na Uingereza (USAID na FCDO). Aidha, Mheshimiwa Rais alifafanua kuwa Tanzania kwa sasa ina mpango madhubuti wa kukabiliana na magonjwa hayo ambapo watu milioni sita kati ya Watanzania wote ndio wapo kwenye hatari ya kupata magonjwa hayo. Hata hivyo, alieleza kuwa jitihada kubwa zinapaswa kufanyika ili kutokomeza kabisa magonjwa hayo. Alifahamisha kuwa licha ya Tanzania kutenga kiasi cha Dola za Marekani milioni 213 bado kuna changamoto na hivyo, uwekezaji zaidi unahitajika. Hivyo, alisihi wadau wa maendeleo kusaidia kutatua changamoto hizo. Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya kuendelea kujumuisha magonjwa yaliyosahaulika kwenye mifumo ya afya ya Tanzania na kuchagiza upatikanaji wa fedha kukabiliana na magonjwa hayo kutoka kwenye vyanzo vya ndani vya Nchi. Hivyo, Mheshimiwa Rais aliahidi kutenga kiasi cha dola za Marekani milioni 3 kukabiliana na magonjwa hayo kwa kipindi cha miaka mitano.
Mafanikio yaliyopatikana kwenye Mkutano huo ni pamoja Bw.Bill Gates aliahidi kuchangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 100 kwenye Mfuko tajwa; Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, kiasi cha Dola za Marekani milioni 100; Serikali ya Sierra Leone, kiasi cha Dola za Marekani laki tano; Serikali ya Belgium, kiasi cha Dola za Marekani milioni 44; na Serikali ya Marekani, kiasi cha Dola za Marekani milioni 114. Jumla ya ahadi zilikuwa ni Dola za Marekani milioni 780. Mambo ya kufuatilia ni pamoja na kufuatilia utekelezaji wa ahadi tajwa ili kuweza kupata fedha kwa ajili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya afya.
Vilevile Mheshimiwa Rais alikutana na watu mashuhuri akiwemo Bw. Michael Bloomberg mmliki wa Vituo vya Runinga vya Bloomberg na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi. Katika mazungumzo yao Tanzania iliomba masaada kwa taasissi ya Blomberg kuendelea kusaidia sekta ya chai nchini na kufadhili awamu ya pili ya miradi ya kuimarisha sekta hiyo hadi kufikia mwaka 2025 kwa kufadhili kiasi cha dola za Marekani milioni 7. Taasisi husika ilionesha nia ya kusaidia Tanzania.
MIKUTANO YA MAWAZIRI
Mawaziri kutoka SJMT nao walipata fursa ya kufanya Mikutano Mbalimbali. Mkutano kati ya Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo alifanya mikutano ifutayo:
- Makutano na Shirika la Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi (United Nations Office for Projects Services -UNOPS)
Katika mkutano huo Mhe. Waziri alilieleza Shirika hilo kuwa ni jukumu la Ofisi ya Umoja wa mataifa ya huduma za miradi (UNOPS) kusaidia Serikali kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Katika mkutano huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb), alikutana na kufanya mazungumzo na Bwana Jorge Moreira da Silva, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN Under-Secretary-General) na Mkurugenzi Mtendaji, Ofisi Kuu, Makao Makuu ya UNOPS; Dalila Alexandra Ramos Moreira Goncalves, Mkurugenzi wa Kanda kwa Afrika; na Bwana Jakob Tuborgh, Mshauri wa Ushirikiano wa Juu, Ofisi ya Kanda ya Afrika. Katika Mkutano huo maazimio yalikuwa ni UNOPS itakuwa tayari wakati wowote kusaidia kuharakisha mchakato wa kuidhinisha na kupatikana fedha kwa urahisi kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuiwezesha Tanzania kujenga uhimili wa haraka na kufikia malengo ya maendeleo endelevu; itasaidia kuwasiliana na washirika mbalimbali na kuongeza wigo wa Tanzania katika kupata ufadhili wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi; na kutoa huduma mbalimbali za kiufundi ili kuwezesha miradi kutekelezeka kwa urahisi na kwa haraka.
- Mkutano na Bw. Mikko Ollikainen, Meneja wa Sekretariat ya Bodi ya Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund)
Mhe. Waziri wan chi alikutana na Sekretariat ya Bodi ya Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund Board Secretariat) ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo, akiambatana na Dkt. Menan Jangu, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, NEMC, alifanya mazungumzo na Bw. Mikko Ollikainen, Meneja wa Sekretariat pamoja na timu yake. Matokeo ya kikao hicho yalijumuisha Sekretaieti ya Bodi wa Mfuko kuahidi kutekeleza maombi yaliyotolewa na Mhe. Waziri kwa haraka: Ripoti ya Mwaka wa kwanza ya mradi wa Bunda kuiidhinishwa, na hivyo fedha zake zitatolewa wakati wowote kuanzia sasa; Ripoti za Zanzibar imeahidiwa itaidhinishwa ndani ya kipindi hiki cha COP28; na hoja za kamati ya mapitio ya maombi ya ithibati kwa NEMC (Accreditation Panel) zimewasilishwa ili kupatiwa majibu.
iii. Mkutano wa Mawaziri kwenye Jukwaa la Utekelezaji Mpango Kazi wa Mifumo ya kuchukua Tahadhari ya Mapema Barani Afrika
Mhe. Dkt. Selemani Jafo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) alishiriki katika Mkutano wa Mawziri kwenye Jukwaa la utekelezaji Mpango Kazi wa Mifumo ya kuchukua Tahadhari ya mapema Barani Afrika (High-Level Roundtable Ministerial Forum for the Implementation of Early Warning for All (EW4All). Matokeo ya Mkutano huo Mhe. Waziri wa Nchi alitoa taarifa kuhusu hali ya Tanzania katika kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema na kujiandaa kutekeleza mpango kazi wa EW4All. Aidha, Mhe. Jafo aliongeza kuwa bado Tanzania inahitaji msaada zaidi ili kuongeza uwezo wa kitaifa, huku akitambua msaada ambao umekuwa ukitolewa na Shirika la Kimataifa la Hali ya Hewa (WMO). Hatua zinazofuata kuhusu Mkutano huo ni kuiweka Tanzania katika nafasi ya kustahiki msaada zaidi kwa kusimamia na kuimarisha mifumo ya tahadhari mapema kwa njia ya utekelezaji mpango kazi wa EW4II. Ni muhimu Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) kuendelea kufuatilia fursa zinazopatikana kutokana na mkutano huu.
- Hafla ya Utoaji Tuzo kwa Mshindi wa Dunia katika Kuhimili Athari za Mabadidiliko ya Tabianchi
Mhe. Dkt. Selemani Jafo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Mkamu wa Rais (Mazingira na Muungano) alishiriki katika Hafla ya utoaji Tuzo ya mshindi wa Dunia katika kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwa jamii za wafugaji nchini Tanzania. Hafla hii ilifunguliwa na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mtaifa, Ban Ki Moon. Pamoja naye, Mkuu wa Sekretariat ya Bodi ya Mfuko wa Kuhimili Mbadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund), Bwana Mikko Ollikainen alihutubia na kuhamasisha jitihada mbalimbali za kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Matokeo ya Hafla hiyo ni kuwa Mhe. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira): alipata fursa ya kufungua tuzo ya mshindi wa Tanzania na kumtangaza mshindi huyo aliyetoka Kampuni ya Pastoral Women’s Council (PWC) yenye ofisi zake mkoani Arusha. PWC iliibuka mshindi wa kwanza kati ya washindani zaidi ya 500 katika kipengele cha “Wanawake katika Uongozi, kwenye mashindano yaliyoandaliwa na Global Centre on Adaptation. PWC ni shirika lisilo la Kiserikali linalofanya kazi, Kaskazini mwa Tanzania likiwa na lengo la kufikia usawa wa kijinsia na maendeleo ya jamii kupitia uwezeshaji wanawake na Wasichana wa Kimasai. Pamoja na hayo, Mheshimiwa Dkt. Jafo alipongeza jitihada zinazofanywa na makundi mbalimbali yanayoshiriki katika kutoa mchango wa kuhimili mbadiliko ya tabianchi nchini Tanzania. Hatua inayofuata ni pamoja na kuhamasisha Mashirika ya Kijamii yanayojihusisha na shughuli za kuhimili mabadiliko ya tabianchi kushiriki katika mashindano haya.
Mkutano ya Mhe. Dkt. Mwigulu. L. Nchemba (Mb) Waziri wa Fedha
Waziri wa Fedha akiwa kwenye Mkutano wa 28, Dubai alifanya mikutano ifutayo:-
- Mkutano na Mkurugenzi wa Benki ya Standard Chartered
Waziri wa Fedha aliweza kufanya Mkutanao na Mkurugenzi wa Benki ya Standard Chartered Bank. Mkutano ulihusu Mfumo Endelevu wa Ugharimiaji Fedha (Sustainable Financing Framework). Matokeo ya Mkutano ni pamoja na Benki ya Standard Chartered kuelezeaa uzoefu kwenye maandalizi ya mfumo endelevu wa ugharimiaji fedha ambayo inaweza kusaidia nchi kuwa na mpango wa kutafuta/ kupata fedha za kugharimia miradi ya mabadiliko ya tabianchi na ya kijamii. Mafanikio tarajiwa katika Mkutano huo ni Benki ya Standard Chartered iliahidi kuisaidia Wizara ya Fedha kukamilisha maandalizi ya mfumo endelevu wa ugharimiaji fedha ambao itaisaidia Serikali kupata fedha kwa ajili ya kugharimia mabadiliko ya tabianchi na miradi ya kijamii kwa hatigungani (social bonds, green/blue bonds). Mfumo huu utakamilishwa mapema mwanzoni mwa mwaka 2024.
Masuala ya kufuatilia ni pamoja na Wizara ya Fedha kushirikiana na Benki ya Standard Chatered kufanya uchambuzi wa takwimu za matumizi kwenye bajeti ya Serikali, mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo ili kukamilisha maandalizi ya Sustainable Financing Framework ya Tanzania. Aidha, sekta zinazohusika na mazingira na jamii zitahusishwa ili kubaini miradi ya kipaumbele. Sekta hizo ni pamoja na Mazingira, Elimu na Afya.
Mkutano ya Mhe. January Y. Makamba (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alishiriki katika mikutano ifuatayo:-
- Mhe. João Gomes Cravinho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ureno
Mhe. January Y. Makamba (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alikutana na kufanya mazungumzo na Mhe. João Gomes Cravinho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ureno, tarehe 2 Desemba 2023 pembezoni mwa Mkutano wa COP 28. Wakati wa Mkutano huo, Mawaziri hao walizungumzia masuala yafuatayo:-
Mhe. Cravinho alirejea ziara ya Mhe. Stergomena Tax (Mb), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa aliyoifanya nchini Ureno mwezi Oktoba 2023. Hivyo, alikumbushia umuhimu wa kukamilisha Mkataba wa Makubaliano (MoU) baina ya Ureno na Taasisi za uwekezaji katika biashara za Tanzania kama vile Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kuendeleza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ili ushirikiano unaokusudiwa uanze ikiwemo masuala ya usafirishaji. Vilevile Waziri huyo alipendekeza uwepo wa majadiliano ya kisiasa (political consultation) baina ya Tanzania na Ureno kwani wakati wa ziara ya Mhe. Tax nchini Ureno alisaini makubaliano kuhusu kuwepo kwa majadiliano hayo.
Mhe. Januari Makamba alimualika Mhe. Cravinho kufanya ziara nchini Tanzania mwanzoni mwa mwaka 2024, itakayotoa fursa ya kukamilisha Hati ya Makubaliano (MOU) husika na kuimarisha ushirikiano wa uwili uliopo baina ya Tanzania na Portugal. Mhe. Cravinho alitaka kujua hali ya usalama ya sasa ya Cabo Delgado, Msumbiji kwa kuzingatia kuwa Waziri Mkuu wa Portugal atatembelea eneo hilo siku za hivi karibuni. Akitoa mrejesho, Mhe, Waziri alieleza kuwa Mozambique ni nchi Jirani na rafiki kwa Tanzania na hivyo, Tanzania ina vikosi vya walinda amani katika eneo la Cabo Delgado chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Alisema kuwa uwepo wa walinda amani hao imesaidia kwa kiasi kikubwa hata hivyo, alipendekeza umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia zaidi kwa kuboresha hali ya kiuchumi na kijamii katika eneo husika kwani chanzo kikubwa cha kukosekana na usalama katika eneo la Cabo Delgado ni jamii iliyopo katika eneo hilo kuhisi kusahauliwa na Serikali ya Msumbiji.
Mhe. Cravinho alifahamisha kuwa katika Mkutano wa mwaka 2022 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika, Portugal ilifanya Mkutano wa pembezoni kuhusu uhamaji, usalama na mabadiliko ya tabianchi. Alieleza zaidi kuwa katika Mkutano wa mwaka 2023 wa Wakuu hao, Taifa hilo pia linatarajia kufanya Mkutano wa pembezoni kuhusu masuala ya fedha na mabadiliko ya tabianchi. Hivyo, aliialika Tanzania kushirikiana na Portgal katika kuandaa Mkutano huo.
Aidha, Mhe. Cravinho alifafanua zaidi kuwa Ureno imeanzisha mpango wa kuingia makubaliano na nchi zinazoendelea ambapo Taifa hilo linapunguza sehemu ya deni kwa nchi hizo ili badala yake fedha hizo zitumike katika kuwekeza kwenye teknolojia za kijani. Akitoa mrejesho, Mhe. Waziri alishauri kuwa ni vyema ombi hilo likaja kwa njia rasmi na kuahidi Tanzania kukubali kuandaa Mkutano huo wa pembezoni kwa pamoja na Ureno. Mhe. Cravinho pia aliwasilisha ombi la Tanzania kuiunga mkono Ureno katika ugombea wa kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2027/2028 katika uchaguzi utakaofanyika mwaka 2026. Ilielezwa kuwa nchi nyingine zinazogombea kwenye nafasi hizo ni Ujerumani na Austria. Akitoa mrejesho, Mhe. Waziri Makamba alieleza kuwa Tanzania itaiunga mkono Portugal kwenye nafasi hiyo na kufahamisha zaidi kuwa itawasilisha mawasiliano hayo rasmi kupitia Waraka wa Kidiplomasia.
Mkutano wa Waziri wa Afya
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) alishiriki katika mikutano ifuatayo:
- Mkutano wa kwanza wa Afya na mabadiliko ya tabianchi ngazi ya Mawaziri wa Afya Nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani.
Kikao hiki kilichotoa umuhimu wa suala la Afya kilifanyika pembezoni mwa kikao cha 28 cha Duniani kuhusu mabadiliko ya tabia nchi. Waziri Ummy aliuambia mkutano huu kwamba, mabadiliko ya tabia nchi, yamesababisha ongezeko la magonjwa ya milipuko na vifo hususani katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara. Mathalani, magonjwa kama kuhara, malaria, dengue na magonjwa yasiyopewa kipaumbele kama usubi, chikungunya, kichocho, matende na magonjwa ya mfumo wa hewa, magonjwa ya aina hii yanatarajiwa kuongezeka kutokana na ongezeko la joto na mvua kubwa au chache zinazoletelezea mafuriko au ukame katika maeneo mbalimbali nchini. Waziri Ummy alitolea mfano wa mafuriko yaliyotokea nchini mkoani Manyara na kupoteza maisha ya watu na wengine kujeruhiwa. Majanga kama ya mafuriko yameonekana kusababisha milipuko ya ya magonjwa ikiwemo kipindupindu na Homa ya matumbo na kueleza kuwa asilimia 88 tu ya wakazi wa mijini ndiyo wanaopata huduma ya maji safi na salama na kwa upande wa vijijini ni asilimia 77 na watu wenye vyoo vya aina yoyote ni asilimia 98. Aidha majanga kama ya mafuriko yamepelekea kuharibu vyanzo vya maji na miundombinu iliyopo na kupelekea upungufu na hatimaye milipuko ya magonjwa.
Mkutano wa Waziri wa Mifugo & Uvuvi
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) alishiriki katika mikutano ifuatayo:
- Kufanya mazungumzo ya ana kwa ana (bilateral meeting) na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Dunia (World Bank), Dr. Martien Van Niewkoop na kujadili kuhusu uchumi wa buluu, kilimo cha mwani na kuharakisha mchakato wa kuanza kwa mradi wa kuboresha maisha ya wavuvi (Tanzania Scaling-Up Sustainable Marine Fisheries and Aquaculture Management Project (TASFAM) ulioko chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Mkurugenzi huyo aliahidi kushughulikia jambo hilo na kuhakikisha kwamba mradi huo unaanza rasmi ifikapo mwezi Februari, 2024.
- Kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini na Mashariki ya Afrika wa Shirika la Hifadhi ya Mazingira (International Union for Conservation of Nature, IUCN) Ndg. Luther Bois Anukur. Kwa pamoja tulikubaliana kwamba Tanzania iingizwe kwenye mradi mkubwa wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi barani Afrika wa Blue Green Wall (BGW) na kwamba Serikali ya Tanzania iwe championi wa jambo hilo. Mazungumzo haya pia yaliwezesha Nchi yetu kupata mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi yenye lengo la kuboresha kosaafu za mifugo kwa mikoa ya Singida na Manyara wenye thamani ya USD milioni 30 (sawa na shilingi bilioni 76). Mradi huu ulikwama kwa kukosekana kwa barua ya Serikali kuonesha nia ya kuuhitaji ambapo barua hiyo niliisaini na kuiwasilisha kwa Mtendaji Mkuu wa Green Climate Fund (GCF) siku moja baada ya mazungumzo.
iii. Kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya WorldFish Dr. Essam Yassin Mohamed. WorldFish ni taasisi ya kimataifa ya kutafiti usalama wa chakula na kufuatilia ustawi wa sekta ya uvuvi duniani ambapo tulikubaliana WorldFish kuleta nchini miradi mitatu (3) ya utunzaji wa matumbawe, ufugaji wa samaki, kilimo cha mwani, kuzuia upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa na kusapoti program ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT-LIFE) na zaidi Wizara itaisaidia WorlfFish yenye makao yake makuu nchini Malaysia, kufungua ofisi hapa Tanzania.
- Kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Ocean Vision Dr. Brad Ack kwa lengo la kutafuta suluhisho la pamoja la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo kupunguza hewa ya ukaa kwa kutumia bahari. Tulikubalina kwamba Wizara yangu iweze kuisaidia Taasisi hii kufungua ofisi na kuleta shughuli zake hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuanzisha kituo cha ubunifu (Innovation Hub) kwa ajili ya kutafuta njia za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
- Kufanya mazungumzo na mwekezaji wa kiwanda cha kusindika nyama nchini cha Tanchoice anayeishi Dubai. Tulijadili hali ya sekta ya nyama nchini na kile tunachotakiwa kufanya ili kuongeza wigo wa soko la nyama la Uarabuni. Tanchoice wanamiliki kiwanda cha nyama katika eneo la Msoga, Kibaha.
Pamoja na mikutano hiyo ya upili, Mhe. Ulega alishiriki mijadala na mikutano mingine ya wazi ikiwemo:
- Mkutano baina ya Tanzania na Malawi kujadili juu ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Songwe (Lower Songwe Basin) ambapo bwawa hilo pia linatarajiwa kutumika kwa shughuli za kilimo, utalii na uvuvi. Mradi huu una thamani ya dola milioni 760 na unatarajiwa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kupunguza matumizi ya mafuta ya diesel kwani umeme utafuliwa kwa nguvu ya maji.
- Mjadala wa kuwawezesha wakulima na wafugaji wadogo wa bara la Afrika kuhimili mabadiliko ya Tabia Nchi kama njia ya kuhakikisha kwamba jamii inakuwa na chakula cha uhakika. Mjadala uliongozwa na Taasisi ya kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI) ambayo Tanzania ni mshirika wake mkubwa.
iii. Mkutano kati ya Wawekezaji na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambapo niliwahimiza wawekezaji kuja nchini kwa kuwa nchiyetu ina fursa nyingi na mazingira ya uwekezaji ni mazuri. Aidha, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, nilikabidhi cheti cha ruzuku (certificate of incentive) kwa kampuni ya Misri ya Elseweedy Electric East Africa ambayo inatarajia kuzalisha vifaa vya umeme hapa nchini na pia imeanza ujenzi wa kongani la viwanda (Industrial park project) katika eneo la Mlandizi, Pwani.
- Alishiriki katika hafla ya kupokea tuzo ya utalii wa baharini iliyotokana na Tanzania kumiliki kisiwa bora na cha kipekee duniani (World Leading Exclusive Private Island) chenye hotel ya hadhi ya nyota tano iliyoko katika eneo tengefu la Kisiwa cha Shungimbili (kinachosimamiwa na Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi). Aidha, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii niliweza kupokea tuzo ya kimataifa ya utalii inayohusu Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuwa hifadhi inayoongoza duniani katika utalii wa mbugani (World Leading Safari Destination) kwa mwaka 2023.
Mkutano wa Waziri wa Maji
Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso(Mb) alishiriki katika mikutano ifuatayo:
Bilateral meeting na Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB) pamoja Wizara ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Malawi kuhusu Ujenzi wa Bwawa la Lower Songwe na Mtambo wa Kuzaliea Umeme wa Megawati 180, kutoa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 460,000 na Kilimo cha Umwagiliaji hekta 6,200, Bwawa hili liko mpakani mwa Tanzania na Malawi na hivyo uendelezaji wake unahitaji ushirikiano wa nchi zote mbili. Kikao kilifanyika tarehe 3/12/2023.
- Bilateral meeting na AfDB kuhusu ujenzi wa Bwawa la Lugoda katika Mto Ndembera litakalotumika kwa ajili ya Kilimo cha Umwagiliaji hekta 3,600, eneo la Madibira Mkoa wa Iringa, kuzalisha umeme Megawati 3 na kutoa maji kiasi kisichopungua mita za ujazo mbili (2) kwa sekunde kupeleka Mto Ruaha Mkuu wakato wa Kiangazi ili uweze kutiririsha maji Mwaka mzima na hivyo wanyama kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Mkuu waweze kupata maji muda wote wa mwaka. Kikao hili kilifanyika tarehe 3/12/2023.
- Kikao na Ofisi ya Misaada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza (Foreign, Commonwealth Development Office – FCDO) kujadili uwezekano wa nchi ya Tanzania kujiunga na Glasgow Declaration on Fair Water FootPrints. Kusaini Declaration hiyo kutaiwezesha Tanzania kunufaika na Mradi wa Kuimarisha Usimamizi wa Maji utakaogharimu Pauni za Uingereza Millioni 39. Kikao hicho kilifanyika Tarehe 4 Disemba, 2023.
- Kikao na GIZ kuhusu kushiriki kwa Tanzania katika Progamu ya Urban Water Catalyst Initiative yenye lengo la kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka za Maji Duniani. Programu hii itafadhiliwa na Serikali za Uholanzi na Ujerumani na kusimamiwa na Shirika ya GIZ na Benki ya KfW zote za Ujerumani. Kikao hiki kilifanyika tarehe 6/12/2023.
- Kikao na WWF kujadili faida ya Tanzania kujiunga na Initiative ya Fresh Water Challenge ambayo ilizinduliwa wakati wa Mkutano wa Maji wa Umoja wa Mataifa uliofanyika New York Marekani Mwezi Machi, 2023. Tanzania ilikubali kujiunga. Kikao hicho kilifanyika tarehe 6 Disemba, 2023.
- Kikao na UNESCO kujadili ushiriano wa namna ya kuendeleza Maeneo Hamsini (50) nchini yanayoweza kuwa na mtandao wa maji chininya ardhi (well field) kwa kila eneo kama sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi. Kikao hicho kilifanyika Tarehe 6/12/2023.
- Kikao na Global Green Fund (GCF) kujadili uwezekano wa kuanza Utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Kupeleka Maji Mkoa wa Simiyu. Awamu ya Pili itahusisha Wilaya za Meatu na Maswa. Kikao kilikubaliana Way Forward ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Simiyu. Kikao kilifanyika tarehe 8 Disemba, 2023.
- Kikao na GEF kujadili Miradi Miwili ambayo imewasilisha huko kwa ajili ya kupata fedha za utekelezaji wake. Miradi hiyo ni ya Mabonde ya Ruvuma na Wami Ruvu. Mradi wa Bonde la Ruvuma umepitishwa na unasubiri kupelekwa kwenye Bodi ya GEFZ Mwezi wa Pili 2024 ili kupata kibali. Mradi wa Bonde la Wamj Ruvu una maoni ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi na kurejeshwa GEF kwa ajili yq kupitiwa tena. Kikao hicho kilifanyika Tarehe 11/12/2023.
MIKUTANO YA MAKATIBU WAKUU
Makatibu wakuu kutoka SJMT walipata fursa ya kufanya mikutano ifuatayo: Mkutano Baina ya Makatibu Wakuu na Sekeratariati ya NDC Partnership;Mkutano na Mtendaji wa Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi; Mkutano wa Ubia wa Viongozi kuhusu Misitu na Mabadiliko ya Tabianchi (Forest and Climate Leaders Partnership); Mkutano wa Tume ya nchi za Visiwa (Small Islands States Commission); Mkutano kati ya Tanzania na Taasisi ya Global Centre on Adaptation (GCA) kuhusu Uwekezaji wa Kuongeza Uhimilivu wa Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika Nchi za Afrika Mashariki;Mkutano wa Viongozi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa;
USHIRIKI WA SEKTA BINAFSI NA ASASI ZA KIRAIA KATIKA COP28
Katika Mkutano wa 28 sekta binafsi na Asasi za kiraia (AZAKI) zilishiriki ipasavyo katika Mkutano huu. Jumla ya Taasisi 340 zilishiriki ikiwemo Benki ya CRDB, Benki ya Kilimo ya Taifa (Tanzania Agriculture Development Bank-TADB na, Benki ya NMB. Asasi na kiraia na sekta binafsi zilikuwa ndiyo sehemu kubwa ya wajumbe wa Tanzania walioshiriki katika mkutano wa 28.Mikutano iliyofanywa na Sekta Binafsi na AZAKI ni pamoja na: Mkutano kati ya taasisi za fedha na Green Climate Fund (GCF) na UNEP; Mikutano iliyohusu Kilimo cha mwani nchini Tanzania na uwezo wake wa kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa, kwa kuzingatia upatikanaji wa kaboni ya buluu.;
MAKUBALIANO YA NCHI WANACHAMA WA MKATABA WA KIMATAIFA KATIKA COP28
Nchi Wanachama wa Mkataba wa kimataifa wa Mab adiliko ya Tabia Nchi COP28 ziliokuwa na makubalianao kumi na moja kama ifuatavyo:
Lengo la pamojala Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na Mwongozo wake ambao unabainisha mwelekeo ambao Jumuiya ya kimataifa inapaswa kufuata ili kuwezesha jitihada za kuhimili mabadiliko ya tabianchi,ikiwemo shabaha za kuwezesha upatikanaji wa raslimali fedha, teknolojia na kujenga uwezo stahiki nazo zimebainishwa.
Uendeshaji wa Mfuko wa kukabiliana na upotevu na uharibifu utokanao na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uundwaji wa Bodi ya ushauri ya Mfuko huo. Katika Mfuko huu wanachama wamekubaliana kuwa Benki ya Dunia itausimamia Mfuko husika kwa kipindi cha miaka 5 na Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa inayoshughuhlikia Majanga (United Nations Office Disaster Risk Reduction- UNDRR) itakuwa Sekretarieti ya Bodi ya Ushauri. Jumla ya kiasi cha takriban USD Milioni 792 zimeahidiwa kutolewa kwa ajili Mfuko huo.
Tathimini ya Kwanza ya Utekelezaji wa Makubaliano ya Paris imekamilika na kupitishwa na mchakato wa kuanza tathmini ya pili umepitishwa. Tathmini hiyo iliangazia masuala ya upunguzaji wa gesijoto ambapo zinahitaji kupunguzwa kwa 43% ifikapo mwaka 2030 ili kuwezesha joto la dunia kutopanda zaidi ya nyuzi joto 1.5°C. Baadhi ya hatua zilizobainishwa kuwa zinahitajika kufikia lengo hilo ni pamoja na: kuongeza matumizi ya nishati jadidifu, kuongeza jitihada za kuachana na matumizi ya nishati chafuzi; kuondoa ruzuku kwa matumizi ya makaa ya mawe; kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na ushirikishwaji wa sekta binafsi na asasi za kiraia. Aidha, nchi wanachama zimekubaliana kuanza kwa tathmini ya pili ambayo itazingatia misingi ya sayansi katika upatikanaji wa fedha, teknolojia, uhitaji wa maendeleo na ushirikishwaji wa wadau katika ngazi za kitaifa na kimataifa
Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi(Green Climate Fund -GCF) umepokea ahadi ya fedha zaidi wakati wa COP 28. Kiasi cha Dola za Marekani 12.8 billion zimeahidiwa kutolewa kwa ajili ya Mfuko huu.
Mfumo wa masoko na usio wa masoko wa biashara ya kaboni – nchi zimesisitiza kuimarisha zaidi mikakati ya taifa ya upunguzaji wa gesijoto na kuimarisha misingi ya matumizi ya soko katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kujenga Uwezo wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi- nchi wanchama zimekubaliana kuwa nchi zinazoendelea zinatakiwa kujengewa uwezo kuhusu mfumo wa utoaji wa taarifa za jitihada zinazochukuliwa katika nchi husika za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama Mkataba unavyoelekeza ikiwemo matumizi ya Mfumo wa uwazi wa utoaji wa taarifa za misaada inayotolewa kwa nchi hizo.
Kuimarisha utekelezaji wa hatua za kupunguza uzalishaji wa gesijoto; Maeneo yaliyowekewa msisitizo ni pamoja na matumizi ya teknolojia na mbinu za asili ikiwemo utunzaji wa mfumo ikolojia ya misitu, bahari na milima vinapaswa kuimarishwa;
Uendelezaji na uhaulishaji wa teknolojia; nchi na wadau wanapaswa kushirikiana katika kuwezesha upatikanaji wa teknolojia na maarifa.
Imeanzishwa Programu ya Vijana ambayo inatambulika chini ya uataratibu wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi ambapo vijana kati ya miaka 18-35 watateuliwa kuendesha majadiliano kwa ajili ya kuimarisha ushiriki wa vijana katika shughuli za mbadiliko ya tabianchi.
Programu ya mpito wenye kuzingatia haki imeanzishwa kwa lengo la kuendesha mijadala ya kutafuta mfumo bora na wenye haki utakaowezesha kipindi cha mpito; na
Majadiliano kuhusu programu ya upunguzaji wa gesijoto yataendelea katika mkutano ujao;
MANUFAA KWA JMT
Kupitia Mkutano wa 28 JMT itanufaika zaidi na fedha za miradi, teknolojia, utaalam na Programu mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo Programu ya Afrika ya Nishati Safi ya Kupikia; programu ya Afya na mabadiliko ya tabianchi; na utekelezaji wa mikakati ya kuimarisha uhimili katika katika sekta ya maji, misitu na Bahari. Aidha, wafanya biashara na wawekezaji wa Tanzania walikutana na wawekezaji kutoka nje ya nchi na kujadiliana kuhusu fursa za uwekezaji kwenye eneo la mabadiliko ya tabianchi ambapo jumla ya taasisi na kampuni zaidi ya 56 zimeonesha nia ya kuwekeza nchini kwa kushirikiana na sekta binafsi nchini.
MKUTANO WA COP 29
Mkutano wa 29 (COP29) umepangwa kufanyika Azerbaijan 11-22 Novemba 2024, na Mkutano wa 30 utafanyika nchini Brazil tarehe 10-21 Novemba 2025.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza
Mhe. Dkt. Selemani Jafo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano & Mazingira)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU USHIRIKI WA TZ KATIKA COP28