Serikali yaendelea kuhamasisha biashara ya kaboni kwa wananchi

Serikali imeendelea kuhamasisha jamii juu ya biashara ya kaboni ikiwa sehemu ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi katika kuhimiza uelewa na ushiriki wa biashara hiyo katika sekta na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme akizungungumza katika Mkutano Mkuu wa Sita wa Chama cha Washauri Elekezi wa Mazingira Tanzania (TEEA) uliofanyika Dodoma Desemba 12, 2024 kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, amesema jukumu la kutunza mazingira ni la wananchi wote.

Bi. Mndeme amesema anatambua kazi nzuri inayofanyika katika uhifadhi wa Mazingira nchini kupitia Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na kaguzi mbalimbali, hivyo analihimiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuendelea kuwasajili washauri eleklezi haraka, kuwasimamia na kuwajengea uwezo wa kufanya TAM.

“Miradi ya maendeleo kama vile nishati, miundo mbinu, miradi ya usafiri na usafirishaji, utalii, maji, kilimo na mifugo yote inahitaji utaalam wenu katika kutathimini athari za mabadiliko ya tabianchi.”

Kaulimbiu katika mkutano huo ilikuwa ikisema ‘Kukuza Tathmini, Miundo, Bidhaa na Mifumo ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi na Mwitikio kwa Uendelevu wa Mazingira nchini Tanzania,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TEEA Mhandisi Emmanuel Hanai ameiomba NEMC, Ofisi ya Makamu wa Rais (OMR) na wadau wengine wa mazingira waendelee kutushirikisha katika maswala mbalimbali ya Mazingira mfano uundaji wa kanuni mbalimbali za mazingira.

“Napenda kuishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ushirikiano wanaotupatia TEEA katika utendaji wetu katika kulijenga taifa letu pia namshukuru Mkurugenzi Mkuu wa NEMC kwa niaba ya baraza kwa ushirikiano mzuri tunaoupata kutoka kwenu katika shughuli mbalimbali za TEEA na Mazingira kwa ujumla.

Mhandisi Hanai ameongeza moja ya changamoto inayowakabili ni pamoja na uelewa mdogo wa wadau mbalimbali kuhusu TAM, Baadhi ya Taasisi za serikali na wadau mbalimbali bado wanatekeleza miradi bila kufanya TAM hivyo kutukosesha fursa ya kushauri namna bora ya kutunza mazingira.

Naye Kaimu Meneja wa Mapitio ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii kutoka NEMC Mha. Luhuvilo Mwamila amesema Baraza kama mlezi wa Wataalam Elekezi limekuwa likifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha idadi ya wataalam elekezi wenye sifa za kufanya kazi za TAM inaongezeka.

“Kuanzia mwaka 2021 maombi ya usajili na utendaji wa Wataalam Elekezi yanafanyika kwa njia ya mfumo na kwa wakati wote wa mwaka tofauti na zamani ilikuwa mara moja kwa mwaka.”

Amesema maombi ya usajili huwasilishwa kwenye Bodi kila robo mwaka kwaajili ya kupata idhini na maombi ya utendaji huchakatwa na kutoa vyeti muda wowote yanapopokelewa.

Related Posts