Serikali yaendelea kuchagiza biashara ya kaboni

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kujifunza na kupata uzoefu kutoka nchi mbalimbali kuhusu fursa zilizopo katika biashara ya kaboni.

Waziri Masauni amesema hayo Machi 12, 2025), katika Mji wa Seoul nchini Korea Kusini wakati wa ziara yake ya kikazi nchini humo ambapo ameambatana na viongozi mbalimbali wa Ofisi ya Makamu wa Rais akiwemo Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi pamoja na Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) Prof. Eliakimu Zahabu.

Amesema Jamhuri ya Korea ni miongoni mwa mataifa makubwa yanaongoza katika mauzo ya masoko ya kaboni duniani sifa ambazo zimehamasisha ujumbe wa Serikali ya Tanzania kufika nchini humo kwa ajili ya kupata uzoefu iliyonayo katika biashara ya kaboni.

“Katika ziara hii ya mafunzo, ujumbe wetu umelenga kujifunza kuhusu sera, sheria na mifumo ya usimamizi ambayo Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini imekuwa ikitumia katika usimamizi wa biashara ya kaboni” amesema Waziri Masauni.

Aidha Waziri Masauni amesema mwishoni ziara hiyo, ujumbe wa Tanzania kupata ujuzi, mbinu na maarifa ya namna bora ya kutumia mifumo ya kisera na kisheria ili kuwawezesha wananchi kunufaika na biashara ya kaboni.

Ameongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea Kusini hautainufaisha Tanzania pekee bali pia utachangia katika kutatua changamoto za kimataifa katika kukuza masoko endelevu ya biashara ya kaboni na usimamizi endelevu wa sekta ya hifadhi ya mazingira.

Katika ziara hiyo Waziri Masauni pia amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Shirika la Mazingira la Korea (K-eco), Lim Sang Jun, pia ametembelea Chuo Kikuu cha Taifa cha Incheon nchini Korea Kusini pamoja na Taasisi ya Kitaifa ya Sayansi ya Misitu.

Related Posts