Wilaya ya Kilosa inatarajia kuvuna mapato ya Sh1.17 bilioni kama gawio baada ya kuhifadhi misitu iliyowezasha uvunaji wa tani za ujazo 545,433 za hewa ya ukaa (kaboni) katika misitu ya vijiji vyake katika kipindi cha 2023 mpaka February 2024.
Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa Wizara ya Muungano na Mazingira, Tanzania inalenga kuingiza dola za Marekani bilioni 1 (takriban Sh2.4 trilioni) kila mwaka kutokana na biashara ya kaboni.
Katika hotuba ya wizara hiyo iliyosomwa bungeni Machi 2024 wizara ilisema, “katika mwaka wa fedha hadi kufikia Machi, 2024 Jumla ya Miradi 24 ya Biashara ya Kaboni ilisajiliwa na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Kiasi cha dola za Marekani milioni 12.63 (Sh32 bilioni) zimelipwa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kama gawio la mauzo ya viwango vya kaboni”.
Kilosa ikiwa miongoni mwa maeneo yanayonufaika halmashauri na vijiji vimeanza kunufaika.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amewataka wakazi wa wilaya hiyo kujikita katika biashara ya hewa ukaa, kutambua kuwa ni moja miongoni mwa njia mkakati za ukombozi kwao kuanzia ngazi ya vijiji na halmashauri.
https://www.instagram.com/reel/DFx–YlNIo3/?igsh=MmpnNGZ2ejQ2aGxw