Dkt. Kijaji: Andaeni wataalamu wa mazingira kubuni fursa za biashara ya kaboni

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amezitaka taasisi za elimu ya juu nchini kuandaa na kuzalisha wataalamu watakaosaidia kubuni na kubaini fursa zitokanazo na uhifadhi wa mazingira ikiwemo biashara ya kaboni.

Dkt. Kijaji amesema hayo leo Julai 9, 2024 mkoani Morogoro wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kwa ajili ya kujitambulisha na kufahamu majukumu mbalimbali ya kiutendaji ya kituo hicho.

Amesema suala la uhifadhi wa mazingira kwa sasa limepata mwitikio na mwamko mkubwa kutoka kwa wananchi walio wengi, hivyo nafasi hiyo haina budi kutumika vyema na wataalamu kubuni mbinu rafiki na wezeshi zenye kuibua zilizopo katika upandaji miti na uhifadhi wa misitu.

“Ushirikiano baina ya Serikali na taasisi za elimu ya juu ni muhimu kwani itahamasisha wananchi kuhifadhi mazingira, tuandae wataalamu kuanzia ngazi ya cheti ili kuwaelimisha wananchi manufaa na faida za upandaji miti na utunzaji wa misitu,” amesema Dkt. Kijaji.

Aidha Dkt. Kijaji amesema elimu ya uhifadhi wa mazingira ikitolewa kwa wananchi itasaidia katika ukuaji wa sekta za kijamii na kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuwa shughuli hizo zitaendeshwa kwa kuzingatia miongozo ya kitalaamu na kuwaletea faida.

Ameongeza kuwa wakati umefika kwa wataalamu kujitokeza na kuandaa mikakati ya pamoja itakayosaidia wananchi kunufaika na fursa mbalimbali zitokanazo na rasimali na sekta za misitu na mazingira ikiwemo uwepo biashara ya kaboni ambayo kwa kiwango kikubwa inatokana na upandaji miti.

“Tuwaelimishe wananchi ili waone manufaa ya upandaji miti kwa kuhakikisha wanaachana na shughuli zisizo endelevu kwa mazingira ikiwemo ukataji miti kwa ajili ya kuni…Juhudi za pamoja zinahitajika ili wananchi waweze kunufaika na uhifadhi wa mazingira hususani biashara ya kaboni,” amesema Dkt. Kijaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa NCMC Prof. Eliakimu Zahabu amesema biashara ya kaboni ni mfumo uliopo katika soko la dunia unaohusisha upandaji na utunzaji wa miti inayodhibiti uzalishaji wa hewa ukaa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, nishati, viwanda na miundombinu.

“Katika kukabiliana na mabadiliko tabianchi, Dunia imeiona haja ya kuendesha biashara ya kaboni..Tumeendelea kutoa elimu kwa jamii na tumeshuhudia wananchi wa Halmashauri mbalimbali nchini wakipata faida ikiwemo miradi ya maendeleo na fedha,” amesema Prof. Zahabu.

Related Posts