Bunge lapitisha Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira

Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira wa Mwaka 2024, leo Februari 12, 2025 bungeni jijini Dodoma baada ya kufanyia marekebisho kadhaa kutoka katika mapendekezo ya Serikali.

Akiwasilisha maelezo ya muswada huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Yusuf Masauni amesema lengo la jumla la marekebisho yanayopendekezwa ni kuiwezesha Sheria hiyo kuendana na Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 na kutatua baadhi ya changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake.

Amesema Ibara ya 3 ya Muswada inapendekeza marekebisho katika kifungu cha 13 ambacho kinapendekezwa kurekebishwa ili kujumuisha masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi katika masuala ambayo yanasimamiwa na Waziri.

”Madhumuni ya mapendekezo ya marekebisho hayo ni kumpa Waziri mamlaka ya kudhibiti na kusimamia masuala ya mabadiliko ya tabianchi. Pia kuhakikisha kuwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi anapata wasaa wa kutoa maoni yake kabla mipango ya kitaifa ya maendeleo haijapitishwa na mamlaka husika,” amesema Mhandisi Masauni.

Akiendelea, amesema kuwa Sehemu ya Tatu ya Sheria inapendekezewa kurekebishwa kwa kuongeza sehemu ndogo ya (e) inayoanzisha Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), kubainisha malengo ya kuanzishwa Kituo na majukumu yake pamoja na kuweka masharti kuhusu uongozi na vyanzo vya fedha za Kituo.

Amesema kituo hicho kilichopo mkoani Morogoro kimeendelea kutekeleza majukumu yake na kutokana na kutokutambuliwa kisheria kinashindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ikiwemo kushindwa kuingia mikataba ya kitaifa na kimatifa na hivyo kukosa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na biashara ya kaboni.

Waziri Masauni ameongeza kuwa kituo kinashindwa kusimamia kwa karibu masuala ya uuzaji na ununuzi wa viwango vya kaboni kwani hakitambuliki kisheria na kwamba kimekuwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais tangu kuanzishwa kwake na hivyo kinategemewa kuendelea kuwa chini ya Ofisi hiyo ili kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi zaidi hususan katika eneo la mabadiliko ya tabianchi na biashara ya kaboni kwa ujumla wake.

Pia, Waziri Masauni amesema vifungu vya 30 na 31 vinapendekezwa kurekebishwa kwa kuviongezea vitengo vya usimamizi wa mazingira vinavyoanzishwa katika wizara na taasisi mbalimbali jukumu la kushughulikia pia masuala ya mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kuhakikisha kuwa Wizara za kisekta zinatekeleza masuala ya Mabadiliko ya tabianchi kikamilifu.

Ameongeza, Ibara ya 13 ya Muswada inapendekeza kuongeza kifungu cha 75A katika Sheria kwa lengo la kuimarisha mfumo wa kitaasisi wa kuratibu masuala ya mabadiliko ya tabianchi ambapo Kamati ya Taifa ya Ushauri wa Mazingira itatambulika kama Kamati ya Taifa ya Mabadiliko ya Tabianchi.

Kwa upande wake Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeonesha kuridhsihwa na marekebisho madogo 11yaliyofanywa katika na Serikali katika Muswada huo.

Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti Mhe. Jackson Kiswaga, Mhe. Agnes Hokororo ili kukidhi matarajio ya Bunge, wananchi na maudhui ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Kamati inaona kuwa

ipo haja kwa Serikali kuwasilisha Miswada ya Sheria mipya itakayowezesha kutungwa kwa Sheria ya kulifanya Baraza la Taifa la Mazingira kuwa Mamlaka pamoja na Sheria ya masuala ya Uchumi wa buluu.

Hivyo, baada ya hatua hiyo Naibu Spika Mhe. Mussa Azzan Zungu amesema baada ya Miswada hiyo kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapelekwa kwa Rais ili iweze kusainiwa na kuwa Sheria kamili.

Related Posts