Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuapisha Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ndogo ya Tunguu, Zanzibar leo Desemba 10, 2024.
Katika sehemu ya hotuba yake Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtaka Waziri Masauni kushughulikia ipasavyo masuala ya Muungano na kuhakikisha kuwa unaendelea kuimarika.
Aidha, kwa upande mwingine Mheshimiwa Rais amemuelekeza Waziri Masauni kushiki kikamilifu katika majukwaa mbalimbali ili kupaza sauti kimataifa kuhusu masuala ya mazingira.
Halikadhalika, amemtaka kuwatumia ipasavyo na kushirikiana na wataalamu waliopo katika Ofisi ya Makamu wa Rais ili kuhakikisha yote haya yanafanyika.
Itakumbukwa kuwa Mheshimiwa Rais alifanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri na ambapo alimteua Mhe. Mhandisi Masauni kushika wadhifa huo akichukua nafasi ya Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ambaye alimteua kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme.