Spika Tulia azitaka nchi zinazoendelea kuchukua hatua mabadiliko ya tabianchi

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema ni wakati sasa umefika kwa Mataifa yanayoendelea kuchukua hatua katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ametoa kauli hiyo leo Novemba 16, 2024 wakati akizungumza na Watanzania wanaoshiriki katika Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika jijini Baku nchini Azerbaijan.

Mhe. Dkt. Tulia amesema kuzungumzia athari za mabadiliko ya tabianchi haitoshi bali kama nchi zinazoendelea hususan Tanzania zinahitajika jitihada zaidi kuhakikisha hifadhi ya mazingira inakuwa endelevu.

Amewahimiza washiriki wa mkutano huo kuyachukua mazuri yote wanayopata wakati wanapokuwa na mikutano ya pembezoni na wadau mbalimbali kisha kuyafanyia kazi wanaporudi Tanzania.

“Nawapongeza kwa maandalizi na ushiriki wenu katika mkutano huu mkubwa na naamini mmekuja hapa mkiwawakilisha Watanzania zaidi milioni 60 na mkirudi nyumbani mtapelekea uzoefu mtakaopata mkiwa hapa,“ amesema.

Aidha, Mhe. Spika amesema kuwa pamoja na changamoto ya athari za mabadiliko ya tabianchi kuikabili Tanzania, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana nayo.

Amesema hatua ya Serikali kupitia kinara wa nishati Afrika na duniani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuisukuma mbele ajenda ya nishati safi ni mojawapo ya hatua za kuhakikisha Watanzania wanahamia katika nishati safi na kuachana na nishati chafu ambayo si rafiki kwa mazingira.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Bw. Martin Chungong ameshauri suala la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi lisiwe la Serikali pekee bali liguse wadau wote.

Amesema kuwa zinahitajika nguvu za pamoja kutoka serikalini na sekta binafsi hatua itakayosaidia katika kuleta matokeo chanya katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu Chungong amesema inatia moyo kuna washiriki kutoka mataifa na sekta mbalimbali wanavyoshiriki katika Mkutan wa COP29 ambao utakuwa ni moja ya njia za kuungana kwa pamoja katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Related Posts