Dkt. Mpango ataka Afrika kuimarisha vituo vya ufuatiliaji kaboni

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ushirikiano wa kikanda katika utunzaji na uendelezaji wa rasilimali kijani barani Afrika, kama vile misitu, madini ya kimkakati na vyanzo vya nishati safi ni muhimu kwa kuwa rasilimali hizo zina mwingiliano wa karibu unaovuka mipaka ya nchi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Utajiri wa Kijani kwa Mataifa ya Afrika uliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa nchi za Afrika kuwa na sera rafiki zinazoendana zitakazowezesha matumizi endelevu na uwekezaji katika rasilimali za kijani barani humo. Amesema ni muhimu kwa nchi za Afrika kuimarisha vituo vyake vya ufuatiliaji wa hewa ya Kaboni ili kuweza kunufaika na biashara ya kaboni ambayo sasa soko lake duniani limefikia thamani ya Dola za Marekani bilioni 900.

Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuwa mstari wa mbele katika

kuchochea mijadala kwenye jumuiya za kimataifa ili kuweza kutambua umuhimu wa rasilimali kijani kuwa sehemu ya pato la Taifa kwa Mataifa ya Afrika. Amesema licha ya Tanzania kuwa na hazina kubwa ya rasilimali kijani pamoja na madini ya kimkakati ambayo ni muhimu kwa mabadiliko kuelekea nishati safi, uhifadhi bionuai, uhifadhi wa kaboni, udhibiti wa uchafuzi wa mazingira na uhifadhi wa rutuba ya udongo lakini bado rasilimali hizo hazijajumuishwa katika pato la Taifa.

Makamu wa Rais amesema Tanzania inaendelea na uwekezaji ili kuongeza upatikanaji wa nishati mbadala kama vile jotoardhi, nishati ya jua na upepo. Ametaja jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukabiliana na nishati chafu ya kupikia ambayo imekua chanzo cha ukataji miti na upotevu wa hifadhi ya kaboni inayopelekea uharibifu wa rasilimali za kijani.

Mkutano huo umewakutanisha viongozi mbalimbali wa Afrika, wadau wa mazingira pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Related Posts