Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametoa wito kwa Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo (CBCC) kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Amesema changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ipo kwa maana hiyo tunatakiwa kuchukua hatua kuona dunia inakuwa salama kutokana na changamoto hiyo.
Dkt. Kijaji amesema hayo wakati wa kikao na Ujumbe kutoka Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo na Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo ulioongozwa na
Waziri wa Utalii na Mazingira wa Serikali ya nchi hiyo ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni hiyo Mhe. Arlette Soudan – Nonault jijini Dar es Salaam.
Aidha, amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, Tanzania imekuja na biashara ya kaboni ambayo pamoja na mambo kadhaa inahusisha upandaji wa miti kwa wingi ambayo hunyonya hewa ya ukaa.
“Sisi kama taifa tumeanza kuchukua hatua kwenye biashara ya kaboni na tunatamani tuungane, tushirikiane na tunufaike kwa pamoja kubadilisha ujuzi ili tufikie malengo, tunahitaji maendele ambayo wenzetu wamepiga hatua huku wakiharibu mazingira na waathiriki wakubwa ni sisi nchi zinazoendelea,” amesema.
Mhe. Dkt. Kijaji amepongeza CBCC kwa kukubaliana namna wanavyoweza kuzisaidia nchi wanachama kupata fedha ambazo tayari zimewekwa katika Mfuko wa Bluu na benki mbalimbali wanazofanya nazo kazi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za utalii na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande mwingine amesema kama mawaziri wanaoshughulikia mazingira wana jukumu la kuhamasisha wananchi watumie niahsti safi ya kupikia badala ya kuni au mkaa ambazo zinatokana na ukataji wa miti holela.
Amesema kwa kutambua hilo tayari Tanzania imeaandaa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia na Rais Mhe. Dkt. Samia aliamiwia na kupewa ukinara ili wananchi wanufaike lengo la kufika asilimia 80 ya kaya kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034 litimie.
Hivyo, amewapongeza wakuu wa nchi kwnye Mkutano wa COP22 kwa kuanzishwa kwa Kamisheni hiyo (CBCC) ili iangalie mabadiliko ya tabianchi na mazingira kwenye Bonde la Congo.